Hadithi Hadithi with Rupal Ganatra

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) & Taasisi ya Usomaji na Maendeleo–Soma

Maadhimisho ya siku ya wapendanao yaani Valentine kwa mrengo wa Kijinsia

Kauli mbiu: “Wantanzania Tupendane Bila Aina Yoyote ya Unyonyaji, Ubaguzi na Ukatili wa Kijinsia”

Maadhimisho ya siku ya wapendao yatafanyika katika viunga vya Mkahawa wa Vitabu Soma Book Café tarehe 16 February 2013, na kushirikisha wanafunzi kutoka shule za sekondari za jirani ambazo ni :Yusuf Makamba;Loyola High School;Mabibo Secondary;Perfect Vision & Sinza Tower Secondary School.

1.0 Utangulizi:Tarehe kumi na nne ya mwezi wa pili kila mwaka, watu duiniani kote husherehekea sikukuu ya wapendao maarufu kama Valentine. Kwa nchi za Afrika na hususan Tanzania, sikukuu hiii ilianza kusherehekewa mwanzoni mwa miaka ya tisini na kushika hatamu katika miaka ya elfu mbili.

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) ni shirika lisilo la kiserikali lenye dira ya kuwa na jamii ya Tanzania inayothamini usawa wa kijinsia, haki za jamii, ukombozi wa Wanawake kimapinduzi. Ni shirika linalotetea na kupigania haki za binadamu, hususani haki za makundi yaliyoko pembezoni, ikiwa ni pamoja na wanawake, watu wanaoishi na ulemavu, wasichana na wavulana.

Mtandao wa Jinsia Tanzania unatoa kipaumbele kwa mtoto wa kike katika kutoa elimu ya Jinsia mashuleni ikiwa na njia mojawapo ya kujenga vuguvugu la ukombozi wa Wanawake kimapinduzi, na zaidi kwa watoto wa kike kuweza kupigania haki zao kwa kupinga mifumo kandamizi iliyojikita, kwenye jamii iliyowazunguka mijini na vijijini.

Vile vile lengo jingine ni kumjenga mtoto wa kike katika misingi ya uongozi mbadala na wenye misingi ya falsafa ya uongozi shirikishi; utambuzi wa kuheshimu haki za binadamu kwa wote, na kupata uelewa wa haki ya afya ya uzazi, uwazi, uadilifu na uwajibikaji binafsi, na wa pamoja, pia kuwa na msimamo thabiti katika kuthubutu kutoa sauti zao kutetea haki na usawa.

2.0 Soma (Shirika la Usomaji na Maendeleo la E&D) ni shirika la kujitolea lenye njozi ya ‘Kuiona Tanzania Ikipambana na Umaskini kwa Kujigeuza kuwa Jamii Iliyokarabuka, Inayothamini Maarifa, Ubunifu na Fikra Huru’. Mchango wake katika kufikia njozi hii ni kwa kuhimiza usomaji kama burudani, utamaduni na nyenzo huru na endelevu ya kujipatia maarifa ya ukombozi.Hii ni pamoja na kubuni shughuli za burudani zinazoibua fikra na mijadala ya kijamii kuhusu changamoto za maendeleo na utatuzi wake. Madhumuni ni kujenga upenzi miongoni mwa waatoto, vijana na makundi yanayokandamizwa; na thamani ya kuchota maarifa yaliyo katika utamaduni wetu na kuyatumia kujikomboa kifikra na vinginevyo; kwa kujijengea uwezo na utayari wa kubadili mstakabali wa maisha yao na jamii yao. Hii ni pamoja na kupambana na mifumo kandamizi kama vile mfumodume na uliberali mamboleo. Inatumia nyenzo za kifasihi na inafanya shughuli zake kwa ushirikiano na taasisi zenye malengo na mitazamo inayofanana kama vile TGNP.

Soma inaamini kuwa simulizi, fasihi na sanaa kwa ujumla ni nyenzo za kiutamaduni zenye nguvu za kusimika mifumo na kuifumua. Simulizi ni utanzu uliofungamana na jamii kwa karne na karne ulimwenguni kote. Kila kizazi huchota kwenye mapokeo simulizi zenye tija katika kukabiliana na changamoto walizonazo, na kuzinyumbua pale panapo haja au kuzalisha mpya. Simulizi hutumika kuburudisha, kufundisha, kukosoa na hata kuraghbisha harakati za ukombozi. Ni utanzu nyumbufu unaochota kutoka kwenye tanzu nyingine kama maigizo, nyimbo, ushairi, ucheshi, vitendawili, metali ,semi na kadhalika, kulingana na mahitaji ya wakati na hadhira na ujumbe. Mwaka huu, kwa kushirikiana na msimulizi wa kimataifa Rupal Ganatra, Soma imeazimia kuanzisha mfululizo wa simulizi shirikishi zenye lengo la kuchochea mabadiliko ya fikra, kuhoji mitazamo na haarakati nyingine za kuleta mabadiliko. Simulizi ya kwanza katika mfululizo huu ni Cucarachita, itakayosimuliwa katika hafla ya Valentine kwa Mtazamo wa Kijinsia iliyoandaliwa na TGNP; na inayowashirikisha wanafunzi wa shule za sekondari.Hafla hii itafanyika kufanyika kwenye viunga vya Mkahawa wa Vitabu Soma; ambao dhima yake ni kuhimiza usomaji kwa burudani, utamaduni na maaarifa. Soma na washirika wake hutumia uga huu kuratibu majukwaa na matukio mbalimbali ya usomaji kama vile klabu za usomaji; uzinduzi, mapitio, na maongezi kuhusu vitabu na fasihi; sanaa za maonyesho, simulizi, ucheshi, ushairi wa jukwaani; matamasha ya vitabu, mijadala na makongamano kuhusu masuala mbalimbali yanayoikabili jamii; pamoja na shughuli nyingine za burudani. Mkahawa wa Vitabu Soma una huduma ya chakula, vinyaji na duka la vitabu.

3.0 Kwanini Tunaandaa Mijadala mbadala Sikuya Wapendanao (Valentine):

Hii ni fursa ya kipekee ya kupeana taarifa, kujadili, na kujengeana uwezo na kuibua mpango wa pamoja wa utekelezaji/ufuatiliaji katika masuala ya kijamii, kiuchumi, na kimaendeleo kwa mtizamo wa harakati za ukombozi wa wanawake kimapinduzi.

Lengo likiwa ni pamoja na kupata ufahamu na uelewa zaidi juu ya siku hii na kutafakari kama inamkomboa mwanamke kimapinduzi au ni unyanyasaji na udanganyifu.

Hali ilivyo sasa, sherehe hizi za siku ya wapendanao (Valentine) zinatumika kupenyeza masula ya utandawazi na kuendeleza sera na mifumo kandamizi, kwa mfano kufanya biashara kama vile kununua nguo nyekundu, maua, zawadi mbali mbali nk, na hata biashara za mapenzi hasa kwa wasichana na watoto wa kike ili waweze kuwaridhisha wapenzi wao.

Wanaume masikini nao hukumbwa na janga hili kwani watahangaika kutafuta pesa ili waweze kuwaridhisha wapenzi wao kwa kuwatoa outing au kuwanunulia zawadi za valentine.

Hali hii imesababisha, Wana ndoa na wapenzi wengi wameachana, mimba zisizotarajiwa na mimba katika umri mdogo zimetukia, maambukizi mapya ya ukimwi, matumizi ya mihadarati na vitendo vingine vingi vya hovyo hovyo.

Katika hili waathirika wakubwa ni wanawake/ wasichana pamoja na wanaume masikini. Utakuta uwezo wa uchumi wa mtu ni mdogo lakini ataishia kununua zawadi ilimradi amridhishe mwenzie ama kama ni mwanafunzi atahangaika kutafuta fedha ama kudunduliza au hata kuuza mapenzi ili apate pesa akanunue zawadi ya mpenzi wake.

Kipindi cha sherehe za valentine utaweza kuona mwanamme mmoja ana ahadi na wasichana wawili hata watatu na utakuta amewapanga kila mmoja na kwake, na yeye haishi kutulia anahangaika ili awaridhishe, pia kipindi hiki utaona jinsi wasichana na Wanawake wanavyoumizwa kimawazo na kisaikolojia ambapo hukimbiwa na mwenzi wake akijifanya ana kazi nyingi au kasafiri kumbe yupo na mtu mwingine. Unyanyasaji wa kijinsia unakuwepo sana wakati huu na utakuta hata mtu huumizwa kimawazo na hata husababisha vipigo.

Ukiangalia historia ya Valentine haipo katika mahusiano ya kimapenzi bali ni kusaidia watu wenye shida mbalimbali kama wajane, yatima na wasio na uwezo.

4.0 Mfumo wa ubeberu na valentine Day

Mabepari na mfumo wa ubepari ambao ambao msingi wake mkuu ni mtaji na utengenezaji wa faida, kupitia unyonyaji wa kiuchumi kwa wale wasio na mtaji; wakawa wameidaka sikukuu hii na kuigeuza dili. Ubepari ni mfumo ambao hutumia fursa zote zinazojitokeza katika jamii ili kutengeneza faida bila kujali ubinaadamu, na Valentine kwao ni fursa!

Ninaposema mabepari hutengeneza faida bila kuangalia ubinaadamu, nina maana kuwa Bepari aliyekomaa yaani beberu ambaye amedhamiria kufanya biashara ya majeneza kwa mfano, na ambaye amewekeza rasilimali nyingi katika biashara hiyo, yuko radhi hata kutengeneza vifo vya watu kama majeneza yake yatakuwa hayapati wateja hata baada ya kuyatangaza sana.

Matokeo ya siku ya valentine kudakwa na mabepari kutangazwa sana, yameifanya siku hii ishike hatamu na kuzidi kufahamika siku hata siku kiasi cha kufanya sikukuu hii kuwa ya pili kwa umaarufu baada ya krisimasi. Hii ni kutokana na takwimu za wauza kadi zenye ujumbe wa valentine ambao wamedai krisimasi ndiyo inayoongoza kwa kuuza kadi nyingi ikifuatiwa na Valentine. Kufahamika huku, kumeenda sambamba na wananchi kuisherehekea kwa namna tofauti. Wapo wanaoisheherekea kwa kukesha wakifanya ngono, wapo wanaoitumia kwa tabia za kifataki, wengine huitumia kwa kukesha katika majumba ya Starehe wakifanya starehe za kila aina, wachilia mbali wale wanaoitumia kupata wapenzi wapya na kuharibu ndoa za wenzao.

Ni katika hali hii uchafu mwingi wa hatari ambao tunaweza kuuita ukatili wa kijinsia umetukia.

KARIBUNI SANA