Kinara Shindano la Hadithi Fupi – Andika na Soma

Nani kuibuka kinara wa shindano la hadithi fupi kwa wanafunzi wa shule za sekondari – Andika na Soma?

Wanafunzi wa Shule ya Jangwani walioshiriki katika hafla ya ugawaji tuzo kwa washindi wa mzunguko wa pili wa Andika na Soma.
Wanafunzi wa Shule ya Jangwani walioshiriki katika hafla ya ugawaji tuzo kwa washindi wa mzunguko wa pili wa Andika na Soma.

Oktoba 10, 2015, shindano la hadithi fupi – Andika na Soma – lilifikia kikomo kwa kuwatunuku vinara wa shindano hilo katika hafla iliyofanyika katika viwanja vya Mkahawa wa Vitabu – Soma. Mwanafunzi Zahara Tunda, aliehitimu masomo yake katika shule ya sekondari ya wasichana Ruvu aliibuka kidedea baada ya kuwabwaga wanafunzi wenzake 307 walioshiriki shindano hilo, katika mzunguko wa pili wa shindano. Hadithi yake aliyoiita Uyoga ilichaguliwa kuwa hadithi bora miongoni mwa majaji watatu.

Mshindi wa mzunguko wa pili, Zahara Tunda akikabidhiwa zawadi ya vitabu
Mshindi wa mzunguko wa pili, Zahara Tunda, akikabidhiwa zawadi ya vitabu

Kama inavyofahamika, safari moja huanzisha nyengine na mwisho wa safari moja ni mwanzo wa safari mpya. Kilele cha mzunguko wa pili kilichochea na kuanzisha mchakato wa mzunguko wa tatu ambao ulifunguliwa baada tuu ya kufungwa kwa mzunguko wa pili kwa kumpata mshindi. Hii ikafungulia njia kwa mwanafunzi mwengine kuvipokea viatu vya Zahara, mshindi wa mzunguko wa pili; na kuibua swali, Ni nani ataibuka kinara katika shindano hili?

andika-na-soma-2016-poster

Swali hili la msingi limeendelea kuziangaisha fikra zetu mpaka sasa. Wanafunzi walioshiriki wamekuwa na shauku ya kutaka kujua iwapo ni wao walioibuka vinara. Hadithi yangu imekuwa ya ngapi? Je nimeshinda? Maswali lukuki wamekuwa wakijiuliza na wengine hata wakituuliza. Hata hivyo hatimae jibu la swali hilo linakaribia kupatikana hivi karibuni.

Kati ya wanafunzi 107 walioshiriki katika mzunguko wa tatu, wanafunzi 20 wamechaguliwa kuingia 20 bora. Taarifa na mawasiliano ya wanafunzi hawa (20) zitawasilishwa shuleni kwao; na wanafunzi kumi (10) kati ya ishirini (20) watakaribishwa – kupitia shule zao – kushiriki kwenye warsha ya siku tano (5) inayolenga kuimarisha stadi zao za uandishi wa kubuni na kuboresha hadithi zao zifikie viwango vya kuweza kuchapishwa.

Kwa pamoja washiriki (wote) wa shindano hili wanakaribishwa kushiriki kwenye hafla ya kilele cha mzunguko wa tatu wa shindano la Andika na Soma – 14/10/2016. Hafla ya kilele itawawashirikisha pia viongozi na wadau mbalimbali wa elimu, na tasnia ya Kiswahili, fasihi na utamaduni; ambapo ratiba ya hafla itajumuisha kusomwa kwa kazi zilizoboreshwa pamoja na ugawaji tuzo kwa washindi. Tuzo zitagawawia katika nafasi tatu. Mshindi wa kwanza, wa jumla, na nafasi za mshindi wa pili na wa tatu zitagawiwa kwa jinsia zote mbili (ke na me). Hivyo kwa ujumla kutakuwa na washindi watano. Shule itakayotoa mshindi wa kwanza nayo itatunukiwa zawadi.

Licha ya kutanguliza shukurani kwa ushiriki wako na kutoa pongezi kwa ushiriki na ushindani mzuri, bado swali letu la msingi linabaki pale pale… Kati ya wanafunzi hawa ishirini (20) ni nani amefanikiwa kuibuka mshindi?

Athumani Waziri, aliekuwa mwanafunzi wa Ndanda, akipokea zawadi ya vitabu baada ya kuibuka miongoni mwa washindi wa shindano la Andika na Soma
Athumani Waziri, aliekuwa mwanafunzi wa Ndanda Sekondari, akipokea zawadi ya vitabu baada ya kuibuka miongoni mwa washindi wa shindano la Andika na Soma

ORODHA YA WANAFUNZI WALIOFANIKIWA KUINGIA 20 BORA:

Makongo Secondary – Dar es Salaam

  • Swedi Shaury
  • Kulwa Abdallah

Ndanda Boys Secondary – Mtwara

  • Said K. Said

Jangwani Secondary – Dar es Salaam

  • Maria Makasi
  • Irene Exavery Kivalu

Benjamin Secondary

  • Buliba Magambo

Machame Girls Secondary

  • Jackline Kisanga
  • Upendo Mseli & Mariam T. Mwenesi (wameandika hadithi moja)

Masama Girls Secondary

  • Diana Ewaldy

Tambaza Secondary

  • Zawadi Suleiman
  • Seif Ibrahim Chekanae

Loyola Secondary

  • Ashiraph R. Mlaga

Kifungilo Secondary

  • Julieth Samson Marwa
  • Eliana Ludovick Swai
  • Irene Ambrose Gindo

Ruvu Secondary

  • Zela Kilawa
  • Bethlove Steven
  • Aneth Mirambo
  • Hellen Natasha Kyatwa

Zanaki Secondary

  • Asha Hassan Malolo