Soma literary Competition 2013/2014 on April 2014

shindano 2013-2014

ANDIKA NA SOMA-SHINDANO LA UANDISHI WA HADITHI FUPI

Shindano la Hadithi Fupi kwa Shule za Sekondari linaratibiwa na Taasisi ya Usomaji na Maendeleo-Soma. Shindano hili hufanyika kila mwaka. Kuanzia mwaka 2014 kilele chake kitaangukia  siku ya vitabu duniani ambayo ni tarehe 23 Aprili au karibu na tarehe hiyo. Siku hii huadhimishwa duniani kote kwa matamasha ya fasihi yanayoendeshwa kwa siku zaidi ya moja katika wiki tarehe hiyo inapoangukia.

Lengo kuu la shindano hili ni kuwavutia vijana kijisomea na kuandika ili yawepo machapisho  ya kutosha yaliyoandikwa na vijana. Vilevile shindano hili ni jukwaa la kuhamasisha jamii kuona umuhimu wa kuhimiza usomaji kwa kuwezesha uwepo wa maktaba za shule na za mitaani/vijijini kama sehemu ya kujisomea na kuibua fikra na mijadala.

Malengo mahususi

  1. Kuhamasisha usomaji miongoni mwa wanafunzi na jamii kwa ujumla;
  2. Kuchangia katika ongezeko la kazi za fasihi zinawavutia vijana ziliyoandikwa na vijana wenyewe;
  3. Kujenga stadi za uandishi wa kazi za fasihi zenye mrengo chanya wa jinsia kwa wanafunzi wa sekodari;
  4. Kuhamasisha jamii, taasisi za kijamii na za binafsi  kupiga jeki juhudi za kuendeleza usomaji nchini;
  5. Kuwawezesha vijana kutoa maoni yao katika masuala yanayowahusu wao na taifa lao;
  6. Kuwatambua, kuwatangaza na kuwatunza vijana kwa kuonyesha weledi katika kazi za ubunifu.

ANDIKA NA SOMA MZUNGUKO WA KWANZA 2012:

  1. Tulipokea hadithi 74 kutoka kwa wanafunzi wa: Machame Girls, Masama Girlls, Visitation Girls, St.Francisca, Masasi Girls, Baobab Girls, Lugalo Sec, Morogoro Sec, Ruvu Girls, Mazinde Juu, Kilalala, Weruweru, Azania, Tambaza, Loyola, Shaaban Robert, St. Anthony, Makongo High School, Jamhuri Sec, Mbagala Kuu Sec, Aboud Jumbe Sec, Taqwa Sec, City High School,
  2. Hadithi kumi bora zilitoka kwa wanafunzi wa: Baobab Girls (3) , Azania(2), Masama Girls (2), Machame Girls (1), St. Francisca (1), na Morogoro Sec (1).
  3. Mchakato wa upimaji ulifuata vigezo vilivyotajwa kwenye tangazo la shindano. Jopo la majaji lilikuwa na watu wanne kutoka katika tasnia mbalimbali zinazohusiana na fasihi na baadhi yao walikuwa na taaluma zaidi ya moja.Taalum zilizowakilishwa ni: ualimu wa fasihi, uandishi, uchambuzi na uhakiki, uhariri na uchapishaji, jinsia na stadi za maisha. Majaji hao walikuwa: Joram Nkya, Rirchad Mabala, Pili Dumea na Elieshi Lema.
  4. Wanafunzi 7 (kati ya 10 bora) walifaidika na mafunzo ya siku 5 ya uandishi  (wote walikuwa wasichana, wavulana 2 na msichana 1 hawakuhudhuria). Wakufunzi wa warsha walikuwa: M.M.  Mulokozi-Profesa wa fasihi ya Kiswahili na mwandishi, Pili Dumea-Katibu Mtendaji wa Mradi wa Vitabu vya Watoto, na Richard Mabala-mwalimu wa fasihi, mwandishi na mwezeshaji wa stadi za maisha kwa vijana kutoka (Mkurugenzi wa TAMASHA–taasisi ya stadi za maisha kwa vijana).
  5. Mshindi wa kwanza, Rehema Jafari(ke) alitoka Baobab Girls. Jozi ya washindi walioshika nafasi ya pili ni Catherine Charles (ke) wa Baobab Girls na Isihaka Issa (me) wa Azania. Jozi ya walioshika nafasi ya tatu ni Irene Massawe (ke) wa Masama Girls na Peter Nzowa(me) wa Azania. Washindi wote hawa walitunzwa  na  kutambuliwa mbele ya kadamnasi katika hafla ya mahafali na utunuku wa tunzo iliyofikishwa kwa umma mpana wa watanzania kupitia vyombo 5 vya habari na kwenye mitandao ya jamii.
  6.  Shule ya Azania na Baobab zilipata tunzo ya vitabu vya maktaba kutokana na m/wanafunzi wao (kushika nafasi ya kwanza  na/au ya pili.

Sasa tumeingia katika mzunguko wa pili wa shindano la Hadithi fupi kwa wanafunzi wa shule za sekondari 2013/2014. Kamati ya shindano inatumia fursa hii kukuomba wewe mdau, au mwalimu kuhamasisha wanafunzi unaowafahamu au wanafunzi wa shule yako kushiriki kwenye mzunguko huu.

Mwisho wa kupokea hadithi ni Tarehe 31 Januari 2014. Washindi wanatarajiwa kutangazwa mwezi Aprili, 2014 katika tamasha la kilele litakalohusisha utoaji wa tunzo. Washindi watapatikana baada ya upimaji unaozingatia vigezo vilivyobanishwa kwenye tangazo. Waandishi wa hadithi kumi bora wataalikwa kushiriki  kwenye warsha ya uandishi itakayowawezesha kuimarisha stadi za uandishi hadithi fupi na novela na kupewa miongozo itakayowasaidia kuboresha hadithi zao. Baada ya kuzifanyia marekebisho na endapo zitafikia viwango, uongozi wa shindano utawasaidia kupata  wachapishaji. Vile vile wataalikwa kuwa wachangiaji kwenye Soma-Jarida la fasihi linalochapishwa na Taasisi yetu. Taasisi pia itafanya juhudi ya kuandaa jukwaa litakalowakutanisha wahitimu (alumni) wa warsha ya uandishi ya Andika na Soma mara moja kila mwaka.

Kwa wakuu wa shule zilizopata tunzo ya vitabu tutafarijika sana kama utatufahamisha kuwa vitabu hivyo vimekuwa na mchango gani  katika kuhamasisha usomaji na kwa namna gani mnavitumia.

Tutumie maoni yako kwa:

Mratibu, Andika na Soma-Shindano la Uandishi wa Hadithi Fupi kwa Shule za Sekondari, S.L.P 4460 Dar es salaam au barua pepe somabookcafe@yahoo.com

Kumbuka: Bango la tangazo hapo juu  linaonesha na kuelezea  mwanafunzi anachopaswa kufanya.