Thubutu Creative Stories

NI LIPI KOSA LANGU

Kiza bado kilishamiri nje. Hapakuwa kumekucha vizuri. Jua lilionekana lingechelewa kutoka, ni saa kumi na moja asubuhi na hapakuwa hata na dalili ya mwangaza. Nilikwisha valia sare zangu za shule tayari kuanza masomo yangu ya siku hiyo. Taratibu nilijiandaa vya mwisho mwisho pasipo kusababisha kelele yeyote maana sikutaka kumuamsha mjomba. Nilipomaliza nilifungua mlango kwa ustadi mkubwa iliusipige kelele maana mafuta ya bawaba nayo yalikuwa yameisha; kisha nikafunga mlango kwa nje na kupenyeza funguo chini ya mlango.

Safari zangu za alfajiri, nje kukiwa na giza totoro, zilisababishwa kwa kiasi kikubwa na safari ya kutoka Msasani mpaka shuleni ambapo nilikuwa nasoma Shule ya Sekondari Yombo Buza. Hakuna rangi sikuiona pindi nilichelewa. Safari yangu huwa pevu kweli kweli. Adha ya kupata usafiri hususani kwa wanafunzi, funga kazi ni foleni ya Morocco, Magomeni, Ilala Boma, Mataa ya Chang’ombe na kisha kubwa kuliko ni ile foleni ya Tazara.

Hata hivyo, nyakati nyingine mimi hudamka mapema ilimradi niepukane na kadhia za mjomba, maana kutwa kucha mjomba hunifanyisha kazi nyingi. Wakati mwengine asubuhi najikuta nikitumikishwa mpaka muda wa masomo kuanza hunikutia nyumbani, hivyo hulazimika kutokwenda shule maana nimekwisha chelewa.Matendo ya mjomba yalinisikitisha sana. Muda mwingi huninyima nauli na pesa ya matumizi. Naamini lengo lake ni kunikatisha tamaa. Hata hivyo mimi hupiga moyo konde na kukazana kusoma.

Vitimbi vya mjomba viliendelea kila kukicha. Kutokana na hali yangu sikuwa na jinsi zaidi ya kuvumilia. Siku moja usiku wa saa nane ambapo nilimaliza kujisomea, usingizi ulinipitia. Ghafla nilihisi kuna mtu ameingia chumbani kwangu. Nikashtuka kutoka usingizini. Mwili wanguulitetemeka. Nilimuona mjomba wangu akiwa uchi wa mnyama akiwa tayari ameshafikia kitanda changu. Nilijaribu kumpiga mateke lakini alinishikilia imara kwa mikono yake, kishaakaweka kidole cha shada mdomoni mwake, ishara ya kunitaka nikae kimya. Mjomba alinibaka bila hata roho yake kumsuta. Alipomaliza aliondoka zake bila kutazama nyuma.

Mapema asubuhi nilipoamka, nilijisikiakama kwamba nimebeneshwa zigo la kuni usiku.Mwili wote uliniuma. Mara nilimuona mjomba. Sura yangu ilijikunja ghafla kama mtu aliyekula nyongo. Mkononi nilikunja ngumi utadhani nipo ulingoni. Lakini cha ajabu, mjomba alinisogelea bila hata kutetemeka na kuniambia… “Ole wako useme hiki nilichokufanyia usiku wa leo.” Nilihisi mwili wangu umeganda, nikaishiwa nguvu. Mdomo wazi, niliduwaa huku machozi yakinitoka bila kizuizi, sura nimeikunja na mwili unatetemeka. Ilikuwa Jumapili.

Jumatatu nilienda shule kama kawaida lakini wanafunzi wenzangu walinishangaa sana.Siku hiyo sikuongea na mtu. Nilibaki nikilia tu huku sura nimeikunja. Sikujisikia vizuri. Nilihisi naumwa.

Niliporudi nyumbani sikumkuta mjombalakini usiku ulipofika alitokea aliendelea na vitendo vyake viovu.Hii iliendelea kila siku. Ndipo nilipoamua hatimaye kuchukua uamuzi wa kwenda kumwambia mwalimu wangu wa darasa. Mwalimu wangu aliamua kwenda kuwataarifu walimu wenzake. Walisikitika sana. Wakaamua kwenda kwenye vyombo vya haki za binadamu kutoa taarifa juu ya unyanyasaji huo. Watu wa haki za binadamu waliduwaa kuona kuwa bado vitendo vya namna vinaendelea.

 

UA LISILOTHAMINIKA

Shamrashamra za sikukuu ya Mei Mosi zilishamiri kila pembe ya mji. Kama ilivyoada,kila mmoja wetu alipenda kutemblea sehemu mbalimbali katika siku hii. Mimi na marafiki zangu tulipanga kwenda kwenye gulio ili kujinunulia vitu mbalimbali. Kiukweli ilikuwa ni siku nzuri sana.

Umati na utiriri wa watu ulifurika mithili ya sisimizi katika gulio la Manzese. Kila mtu alikuwa anaendelea na shughuli zake. Vikumbo na zogo zilitawala. Ghafla, shangwe lote lililotanda pale lilinipotea baada ya kuhisi kitu kikipita kiunoni mwangu. Mwili unikisisimka. Vinyelea vilinisimama mwili mzima. Hisia zangu zilinipeleka mguso ule unapotokea. Macho yalinitoka mithili ya mjusi aliebanwa na mlango nilipoona mkono ukipita katika kiuno changutaratibu kuelekea kifuani mwangu. “Mama!” niliupigilia mbali mkono ule na kuutoa kiunoni mwangu.

Marafiki zangu waligeuka na kunitazama baada ya kusikia kilio change. Wakati huo sura yangu ilishaanza kuumuka. Macho yalinitoka kama mtu aliyetafuna pipili mbuzi. Nilirusha keleb ya nguvu ikapata yule kijana pima usoni na hapo hapo nikamkwida. Wakati nikiendelea kukurupushana naye, baadhi ya watu waliokuwa wamenizunguka wakaanza kumtetea. “Dada na wewe unachura kubwa. Yaani limesimama haswa.” Hapo hapo yakaibuka majibizano baina ya pande mbili. Upande mmoja wakipinga vikali kile kitendo nilichotendewa na wengine wakikubaliana na kitendo cha yule kijana. Kisa, maumbile yangu.

Marafiki zangu walinitoa eneo lile na tukamuacha yule kijana kwenye ule umati akiendelea kushughulikiwa na wananchi. Nilipofika nyumbani nilimuelezea Mama yaliyonisibu. Alinipa pole na kunisihi endapo kitendo hicho kitajitokeza tena nisikimbilie kudondosha machozi bali nithubutu kunyanyua mdomo wangu na kutetea haki yangu kwa kuwa ni udhalilishaji kufanyiwa jambo kama hilo.

Tangu hapo nilijaribu kusema kilichomo moyoni mwangu kwa watu wote waliowafanyia wasichana vya hovyo. Nilianza kukemea vitendo vya uzalilishaji shuleni,nyumbani,barabarani hata kwenye magari. Hatimaye nikajikuta nimewasaidia wenzangu wengi kwa kuwa nimethubutu kusema yaliyomo kwenye mioyo yao.

 

VIJIMAMBO VYA SOKONI

Siku moja mimi na dada yangu aitwaye Amina tulikwenda sokoni kununua vitu mbalimbali. Dada Amina ni mrefu na mwenye mwili kidogo; ana mwili wa kibantu haswa, amejaza kote, ila mimi ni mrefu wa wastani. Nimebarikiwa mwili mdogO tofauti na wake.

Siku hiyo tulipokwenda sokoni Tandika, katika pitapita zetu kwenye maeneo ya mitumba,tuliona sehemu imejaa watu wengi sana kiasi kwamba waliziba njia. Bila shaka, kutokana na wingi ule, hata mtu akikukanyaga usingeweza kusema kitu. Sehemu moja hata hivyo ilikuwa imejawa na watu wengi vilivyo nasi kwa shauku ya kutaka kujua yanayoendelea tuliamua kusogelea eneo lile ili tuone kuna nini.Tuliona wacheza singeli wakitumbuiza kwa nyimbo zao mbalimbali huku wakicheza na kunengua utadhani viuno vyao havina mifupa.

Tulinogewa na kusogea karibu zaidi, tukaanza kuchagua nguo na vyombo mbalimbali vilivyokuwa vukiuzwa pale. Dada yangu alisogea upande mwingine na kuendelea kuchagua nguo. Wakati akiwa anachagua nguo mara alisikia mguso usio wa kawaida katika mgongo wake, mara akaona mikono migumu mithili ya ngozi ya mamba ikigusa kifua chake na maziwa yake, alishindwa kuongea chochote. Aliacha mdomo wazi kama anataka kumeza nzi, huku akitetemeka na kutoka jasho. Akaamua kugeuka nyuma na kumuaona mfanyabiashara akiendelea kumpapasa. Dada alikunja uso na kung’ata meno yake,kisha akampiga kibao cha nguvu usoni,hajakaa vizuri akampiga cha pili na cha tatu. Yule mfanyabiashara alijikuta amekunjwa kama mwizi.

Watu wengi walijaa na kutaka kujua kulikoni wengine walizomea na kurusha mawe. Taharuki ile iliendelea kwa muda na mara polisi wakafika na kumchukua yule mfanyabiashara akiwa amejeruhiwa vibaya sana. Polisi wakampeleka kituoni na alifunguliwa mashtaka ya udhalilishaji wa kijinsia na kesi yake inasikilizwa katika mahakama ya mwanzo.

 

MKE WA BABA

Kuondoka kwako mama kumeniachia jeraha kubwa maishani mwangu. Daima ulikuwa nguzo yangu na majibu ya maswali yangu.Sasa nimebaki mkiwa kama njiwa juu ya paa.

Tegemeo langu limekuwa jipu kooni.Uliyeniacha naye amegeuka kuwa nyuki ndani. Siku chache zilizopita baba alinituhumu kuwa niko kwenye mahusiano na kuniwekea sanduku la kondomu chumbani kwangu.

Nilipata donge kooni, lililoyeyushwa na maji yaliyomiminika kutoka machoni kwangu. Nilipomwomba shangazi anisaidiea alilirudisha donge kooni kwangu kwa kuniambia; “Huyo ni baba yakona kaka yangu, mimi ninajua fika hasemi uongo na kama ni mwongo basi mvumilie.”

Nilipofika nyumbani hali ilikuwa si shwari kwani baba alikuwa ameshapata taarifa kutoka kwa shangazi. Nilimkumbuka sana mama yangu kipenzi nilitamani uwepo wako maishani mwangu japo kwa siku moja tu.

Kishindo cha nguvu kilinishtua na kunirudisha kizimbani. Ghafla nilimwona baba na kijana nisiyemfahamu waking’ang’ana kunivua nguo na kuniambia nisipige kelele. Nilipoamka baba aliniambia nikisema utakuwa ndio mwisho wa maisha yangu. Tangu siku hiyo niliendelea kumuachilia baba aingie chumbani kwangu kila alipotaka ili kulinda maisha yangu.

Leo hii nakulilia mama yangu, baba yangu amenivisha pete ya maisha. Pumzika kwa Amani mama,japo amani yangu umeondoka nayo.

 

SITOSAHAU

Ni vigumu kusahau,yale yalliyonitokea,
Juu ya unyama huu, kovu ulilonitia,
Vijana wenye makuu, tena waliokomaa,
Ubaya walinitenda, bila hata ya huruma,

Ilikuwa ijumaa, asubuhi na mapema,
Shuleni naelekea, mara ghafla kasimama,
Nyuma nikaangalia, thibitisha usalama,
Mara wakanivamia, vijana walokomaa.

Kwa nguvu kunikamata, jumba bovu kuniweka,
Kelele wakanikata,kwa manguo nipachika,
Na chini wakanitupa, na kuanza kunibaka,
Sana nilitapatapa, ila sikuchoropoka.

Nilishindwa kutembea, kujikaza chechemea,
Watu wakanishangaa, vidole nilinyooshewa,
Chini niliinamia, machozi yakanijaa,
Nilijawa na uchungu, kwenye maji ya kifuu,


Niliwaza akili, wapi pa kuelekea,
Na ndipo nikabaini, polisi patanifaa,
Nilisema kwa yakini, hata wao wakalia,
Hatua wakachukua, wahalifu fatilia,

Nilienda zahanati, kupima kama ni kwema,
Maibu kama mtiti, nikashindwa kuhema,
UKIMWI ni kizingiti, kilinirudisha nyuma,
Kwa mawazo nilikonda, kabla ya kujikubali,

Kupita miaka miwili, hukumu ilitolewa,
Miaka kumi na mbili, jela walihukumiwa,
Na faini laki mbili, kitwani ililipwa,
Kidogo nilifurahi, machungu yakapungua.

KICHAKA

Nakichukia kichaka,
Cha majani marefu
Na majani mafupi,
Ndoo iliyoniporomoka,
Na nguo zilizochanika,
Kama panya wamepita.

Mtama nikaula,
Nachini nikawekwa,
Heshima nikashushwa,
Kwa mambo yalofanyika,
Kilio kikasikika,
Hakuna aliyeitika.

Nyumbani kufika,
Mjinga nikapikwa,
Shada la kijitakia
Nalo nikawekwa,
Hakika nimedhalilika,
Roho sina pakuiweka.

Hiyo ndo dunia,
Majanga kawaida,
Mama vumilia,
Wanaume si unawajua?
Maneno ya kunipoza,
Wakubwa wanakuhusia.